24 Jul 2024 / 93 views
De Bruyne kubakia Man City

Meneja wa Manchester City Pep Guardiola amesema kiungo mwenye ushawishi mkubwa Kevin de Bruyne atasalia katika klabu hiyo.

De Bruyne amekuwa akihusishwa pakubwa na kuhamia Saudi Arabia majira ya kiangazi.

Amebakiza mwaka mmoja katika mkataba wake wa Blues na alisema mwezi uliopita atalazimika kufikiria ofa kutoka kwa Ligi Kuu ya Saudia kwa sababu ya "fedha za ajabu" zilizopo.

Hata hivyo, Guardiola hana wasiwasi. "Kevin haondoki," aliwaambia wanahabari kabla ya mechi ya ufunguzi ya timu yake ya kabla ya msimu mpya dhidi ya Celtic huko Chapel Hill, North Carolina.

De Bruyne aliisaidia City kunyakua taji la Ligi Kuu msimu uliopita, likiwa ni la nne mfululizo katika klabu hiyo na la sita kwa jumla katika klabu hiyo.

Kiungo wa Crystal Palace wa timu ya taifa ya Uingereza ya Euro 2024, Eberechi Eze amehusishwa na kuhamia City, huku kipa wa Brazil Ederson pia akiwindwa na Saudi Arabia.

Lakini Guardiola anahisi kuna uwezekano mkubwa atakuwa na kikosi sawa na msimu uliopita. "Ikiwa mtu ataondoka, tutazungumza juu ya hilo na, bila shaka, hadi siku ya mwisho [ya dirisha la uhamisho] tuna nafasi," alisema.

"Sikatai wachezaji wapya kama chaguo, lakini nadhani kuna nafasi ya 85, 90, 95% tutakuwa na kikosi sawa." City wataanza kutetea taji lao la Ligi Kuu dhidi ya Chelsea mnamo Agosti 18.